Advertisement

Responsive Advertisement

JEURI YA FEDHA SIMBA SC, PHIRI AFIKISHIWA HOTELI LA BEI MBAYA DAR, ATAIGHARIMU KLABU SH 400,000 KWA USIKU MMOJA TU

Hoteli la bei chafu; Kocha Patrick Phiri kulia akisaini kitabu cha kuingi chumba katika hoteli ya Regency. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Collins Frisch

KOCHA Patrick Phiri amefikishiwa kwenye hoteli ambayo gharama ya chumba chake ni dola za Kimarekani 120 (karibu Sh. 200,000 za Tanzania) kwa siku- na wakala wake pia, amechukuliwa chumba cha hivyo.
Maana yake, malazi ya Phiri katika hoteli ya Regency, Dar es Salaam pamoja na wakala wake yataigharimu Simba SC wastani wa Sh. 400,000 kwa siku.
Phiri anaweza kusaini Mkataba kesho na baada ya hapo wakala wake atarejea Zambia, naye kuendelea kuishi katika hoteli hiyo- na atapewa usafiri pia. 
Haijulikani mshahara wa Phiri utakuwa kiasi gani, lakini mara ya mwisho aliondoka Simba SC akiwa analipwa dola za Kimarekani 5,000 (zaidi ya Sh. Milioni 7.5) kwa mwezi. 
Phiri amepokewa mchana wa leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na kuwekwa kwenye gari la wazi juu akipitishwa mitaa ya Jiji la Dar es Salaam ili manazi wa timu hiyo wamuone, kabla ya kufikishwa Regency Hotel.
Kocha huyo bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2009/2010, kesho anatarajiwa kusaini Mkataba wa kuifundisha klabu yake hiyo ya zamani, Simba SC, akirithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic aliyefukuzwa mwishoni mwa wiki.
Mzaliwa huyo wa Mei 3 mwaka 1956, alifanya kazi kwa awamu tatu tofauti akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kati ya mwaka 2004 na 2010 na kwa mafanikio makubwa- na sasa anataka kurejesha enzi za wana Simba ‘kutembea vifua wazi’.
Mmemuona?Kocha Phiri akipitishwa mitaa ya Dar es Salaam
Kocha Phiri kulia akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Said Tuliy kushoto
Mzambia huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba SC, misimu ya 2004/2005 na 2009/2010 na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 la Tanzania na Kenya.

Phiri ni kocha anayekubalika zaidi mbele ya mashabiki wa Simba SC miongoni mwa makocha waliowahi kufundisha klabu hiyo- rekodi yake ya kukumbukwa zaidi ikiwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009/2010 bila kufungwa hata mechi moja.
Lakini pia, namna alivyoweza kuiongoza Simba SC kuwatambia watani wa jadi, Yanga SC ni jambo lingine linalomfanya awe kocha mwenye heshima ya kipekee Msimbazi.
Katika awamu zote tatu alizofundisha Simba SC awali, Phiri hajawahi kufukuzwa- kwani amekuwa akiondoka mwenyewe kwa sababu mbalimbali.
Kwa sasa, mume huyo wa Cecilia Mutale waliyezaa naye watoto wawili, Melesianiah na Patrick Junior, anarejea Simba SC akitokea Green Buffaloes ya Ligi Kuu ya Zambia.
Phiri ni kocha mwenye mafanikio tangu anacheza soka katika klabu za Rokana United (sasa Nkana F.C.) na Red Arrows zote za nyumbani kwao, Zambia kama mshambuliaji.
Alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na 1982, kabla ya kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana. 
Akiwa kocha, Phiri pia aliiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia kucheza Fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia nchini Nigeria mwaka 1997 kabla ya kushinda tuzo ya kocha bora wa mwaka nchini mwake mwaka 1999.
Simba SC Jumapili ilivunja mkataba na Mcroatia, Zdravko Logarusic ikiwa ni siku moja tu baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Loga ambaye aliongezewa Mkataba wa mwaka mmoja mwezi uliopita- inadaiwa amefukuzwa kwa sababu za kutotii miiko na maadili ya klabu na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva alisema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kumvumilia kwa kiasi cha kutosha.
Loga ameondoka Simba SC baada ya kuiongoza katika mechi 21 tangu Desemba mwaka jana, kati ya hizo akishinda nane, sare tano na kufungwa nane.
Loga aliyerithi mikoba ya Mzalendo, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’, aliikuta Simba SC bado ipo kwenye mbio za ubingwa msimu uliopita, lakini mwishowe ikamaliza nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City, Yanga SC na Azam FC mabingwa.

Post a Comment

0 Comments