Advertisement

Responsive Advertisement

UKAWA Wajitoa Rasmi Kwenye Mchakato wa Katiba, Wanazuoni Wawapa Somo.


KAMA ndivyo, huenda Bunge Maalumu la Katiba, linalotarajiwa kuanza awamu ya pili ya vikao vyake kesho kutwa mjini Dodoma, litafanyika bila ya kuwa na wajumbe kutoka kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Hali hiyo inatokana na kauli ya Ukawa, inayoundwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na wafuasi wao, kwamba hawatashiriki katika Bunge hilo na kwenda mbali zaidi, wakidai hawana mpango wa kuwa na vikao vya maridhiano dhidi ya wenzao wa chama tawala, CCM baada ya kikao kingine cha juzi, kilichokuwa cha nne, kukwama.

Kauli ya Ukawa ilitolewa jana, mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda umoja huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia. Kwa pamoja, walisema wameridhia kujiweka kando katika Bunge na vikao vya maridhiano. Chama cha NLD kinachoongozwa na Dk Emmanuel Makaidi, nacho kimejiweka kando.

Mbowe alifafanua kuwa baada ya kikao cha nne cha maridhiano kati ya umoja huo na CCM, kilichofanyika juzi chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuvunjika, wametafakari kwa kina na kubaini kurejea bungeni kuendeleza mivutano, hakutakuwa na tija kwa Taifa.

“Hivyo tumeazimia kutorejea tena katika Bunge la Katiba wala kushiriki mazungumzo yoyote kuhusu suala hilo, kutokana na ukweli kuwa mazungumzo haya yaliyovunjika, yalikuwa ya kuwezesha kupata Katiba bora, lakini CCM waliyafanya kuwa yenye maslahi ya chama chao, siyo Taifa.

”Na baada ya awamu nne za vikao vya mazungumzo kati yetu na CCM, Ukawa tunatangaza kwamba hatuko tayari kuendelea na mazungumzo na CCM wala kurudi katika mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti maoni ya wananchi na kutumia vibaya fedha za umma,” alisema Mbowe.

Kauli ya CCM Hata hivyo, kwa mara nyingine jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema chama chake hakijashangazwa na uamuzi huo, kwa kuwa walifahamu Ukawa hawana hoja za msingi, hivyo wamekimbia aibu.

“Hata kwenye vikao, hawakuwa na kitu kipya, ni malalamiko tu huku wakishindwa kujenga hoja, kwa hiyo tulijua hawa wenzetu lazima mwisho wa siku wakimbie aibu yao…ni aibu tu imewashika, ndiyo maana wamepatafuta pa kutokea,” alisema Nnauye.

Wakati huo huo, Mkuu wa Shule ya Sheria nchini Kenya, Profesa Patrick Lumumba amewasihi wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwa itakuwa si busara kutorejea bungeni Agosti 5, mwaka huu, badala yake watumie nafasi hiyo kurudi bungeni na kushindanisha hoja zao.

Alisema hayo katika mdahalo wa kutoa maoni na msimamo wa wananchi, juu ya mivutano ya makundi katika mchakato wa Katiba. Mada mdahalo huo ilikuwa ni “Nini suluhisho na wajibu wa makundi katika mchakato wa Katiba”.

Mdahalo huo ulitayarishwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS). Ulifanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, jana.

“Katiba ni ya Watanzania, siyo wanasiasa wa Tanzania, wale waliomo ndani ya Bunge la Katiba ni wajumbe tu ambao wametumwa, kwa maana hiyo hata kama ni wanasiasa wako kule ni lazima wasahau vyama vyao na kuupa kipaumbele Utanzania wao,” alisihi Profesa Lumumba.

Alisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee na kihistoria barani Afrika ya kupata Katiba mpya, bila mapigano ya aina yoyote. Alisema litakuwa ni jambo la kushangaza na kusikitisha, ikiwa amani iliyopo hivi sasa, itatumiwa na wanasiasa wenye ufinyu kwa mitazamo yao ya siasa na kusababisha mapigano.

Profesa Lumumba alisema Rais Jakaya Kikwete aliona umuhimu wa Tanzania, kuwa na Katiba mpya na aliamua kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba hiyo.

Profesa huyo alisema Rais Kikwete anastahili kupongezwa na kila mtu, kwa hatua yake hiyo kubwa na nzuri kwa Taifa la Tanzania.

Alisema Tanzania inatakiwa kujifunza kuhusu uandikaji wa Katiba mpya, kutokana na makosa yaliyofanywa na nchi nyingine, ambako yalitokea mapigano

Post a Comment

0 Comments