KATIKA hali isiyo ya kawaida, baadhi ya wakazi wa Tegeta, Dar es Salaam, wamekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpitisha Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli awe mgombea wa chama hicho kwenye nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, kutokana na uchapakazi wake kwenye sekta ya ujenzi wa barabara nchini.
Wakazi
hao walitoa ushauri huo jana wakati Dkt. Magufuli akiwa na Mkuu wa Mkoa
huo, Bw. Said Meck Sadick wakikagua barabara ya Mwenge-Tegeta, ambayo
ujenzi wake umekamilika.
Katika
ukaguzi huo, wakazi hao baada ya kumwona Dkt. Magufuli, walianza
kumshangilia na kusema anafaa kuwa Rais kwa tiketi ya CCM katika
Uchaguzi Mkuu 2015.
"Mheshimiwa
wewe unafaa kuwa Rais, hongera sana kwa kutupunguzia foleni kwani una
chapakazi...hakuna mwingine zaidi yako lakini barabara hii haina taa
hivyo tunaomba utuwekee," walisema.
Akizungumza
na wananchi hao, Dkt. Magufuli alisema maendeleo hayana itikadi ya
chama chochote cha siasa wala dini bali ni ya watu wote ambapo miradi
yote ya ujenzi wa Barabara katika jiji hilo itagharimu sh. trilioni moja
hadi kukamilika kwake.
Alisema
kazi hiyo inafanywa na Rais Jakaya Kikwete kutoka na ushirikiano mzuri
uliopo na mataifa mengine na barabara hiyo ataizindua mwenyewe kabla ya
kuondoka madarakani ili asije Rais mwingine akasema yeye ndiye
aliijenga.
"Baada
ya miaka mitatu, jiji la Dar es Salaam halitakuwa na foleni tena kwani
hivi sasa, barabara hii imekamilika kwa gharama ya sh. bilioni 89,
katika bajeti ya mwaka huu, tumetenga sh. bilioni 2 ili kuiwekea taa
ila daraja lina uwezo wa kuhimili tani 180 lakini mnapaswa kutambua
kuwa, hakuna vitamu bila uchungu," alisema Dkt. Magufuli.
Aliongeza
kuwa, mbali ya barabara hiyo upanuzi wa Ujenzi wa Barabara ya Mwenge
hadi Morocco, nao uko mbioni kuanza na ile ya kutoka Bagamoyo hadi
bandarini ipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuanza kazi ili
kupunguza msongamano.
"Tupo
katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa barabara za juu, kutakuwa na
barabara za ghorofa tatu zinazopishana pale Ubungo na Tazara ambako
ujenzi wake utaanza Oktoba mwaka huu, nyingine itakuwa Kamata, lengo ni
kupunguza foleni," alisema.
Kwa
upande wake, Bw. Sadick aliwaonya watu wanaohujumu miundombinu ya
miradi ya Barabara baada ya kupewa taarifa kuwa sababu zinazosababisha
Mkandarasi wa Barabara ya Mabasi yaendayo Kasi (DART), kushindwa
kuikabidhi ni kutokana na watu kuiba taa.
Alisema
hadi sasa, taarifa alizopewa taa saba na mabomba yake yameibwa ambapo
mifuniko ya maji mchafu 12 na alama za barabara 25, nazo zimeibwa na
watu wasio waaminifu.
"Ni
marufuku kwa mtu yeyote kufanya biashara eneo la barabara ya mradi huo
au kupumzika katika vituo vya mabasi haya...miradi hii inatumia fedha
nyingi lakini watu wachache wanataka kuturudisha nyuma," alisema Bw. Sadick.
Naye
Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada alisema Serikali ya nchi yake
itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya barabara ili kupunguza tatizo
la foleni nchini.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale,
alisema baadhi ya miradi ya barabara inakwamishwa na watu ambao tayari
wamelipwa fidia lakini wanadai fidia waliyolipwa ni ndogo.
0 Comments