MENEJA
wa Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni, Alune Kasilika, amedaiwa kuwa
aliwasiliana na watuhumiwa wa tukio la ujambazi katika benki hiyo
wakiandaa utekelezaji wake.
Hayo
yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa
Serikali, Janeth Kitali, mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulile Mwaseba, wakati
akiwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Kitali
alidai siku ya tukio Aprili 14, mwaka huu, mshtakiwa Alune na Neema
Batchu ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo, walifika kazini na shughuli
za kibenki ziliendelea pamoja na wafanyakazi wengine.
“Mheshimiwa
hakimu, mshtakiwa wa kwanza ambaye ni meneja wa benki hiyo, Alune, siku
ya tukio alikuwa na mawasiliano na mshtakiwa wa tatu hadi wa kumi ili
kuandaa tukio la wizi wa fedha za benki hiyo na hatimaye lilifanyika,” alidai.
Alidai
kuwa wizi ulifanikiwa baada ya washitakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa
benki hiyo kutoa taarifa za kina kuhusu benki kwa mshtakiwa wa tatu hadi
wa kumi.
Aidha,
alidai kuwa Sajini Iddi na Bundala wakati upelelezi wa kina ukifanyika
huku wakijua mshtakiwa wa kwanza hadi wa kumi wanatafutwa kwa wizi,
waliwapa taarifa za kiupelelezi ili kuwasaidia wajifiche wasikamatwe na
walikimbia kukwepa mkono wa sheria.
Baada ya kumaliza kuwasomea maelezo hayo, washtakiwa walitakiwa kujibu wanayokubali na wanayokataa.
Hata hivyo, washtakiwa wote walikubali majina yao na walikana maelezo yote yanayohusu wizi huo.
Hakimu Mwaseba aliahirisha kesi na kupanga kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka Septemba 17, mwaka huu.
Kitali
aliwakumbusha washtakiwa mashtaka yao ambapo alidai mshtakiwa wa kwanza
hadi wa tisa, wanashtakiwa kwa kula njama kutenda kosa la wizi wa fedha
za Benki ya Barclays.
Inadaiwa
Aprili 15, mwaka huu kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, washtakiwa
waliiba Sh 390,220,000, Dola za Marekani 55,000 na Euro 2,150 mali ya
benki hiyo na kabla ya kufanikisha wizi huo, walimtishia kwa bastola
Anifa Ahmed na Anna Tegete.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo.
Katika shtaka la mwisho, Wakili wa Serikali alidai linawahusu maofisa wa polisi, Sajini Iddi na Bundara.
Maofisa
hao wanadaiwa kuwasaidia washtakiwa kutoroka ili wasikamatwe na
kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Hata hivyo, walikana pia.
Washtakiwa
katika kesi hiyo ni mameneja wawili wa benki hiyo, Alune Kasilika (28),
Neema Batchu (26), mfanyabiashara Hamis Shabani au Carlos (34), mkazi
wa Magomeni na dereva Manase Genyeka au Mjeshi (35), mkazi wa Tabata.
Wengine
ni wafanyabiashara Kakamie Julius (32), Iddy Khamis (32), Sezary
Massawe (31), Boniphace Muumba (29), Ruth Macha (30) na maofisa wawili
wa polisi, Sajini Iddy (33) na Bundala (37).