Mtoto
Lowassa Kivuyo (14), amelazwa katika Hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Center, baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu na
kumkata vidole tisa vya mikono yake.
Akizungumza
kwa tabu katika hospitali hiyo, mtoto huyo alisema tukio hilo
lilitokea Jumapili Septemba 7, mwaka huu saa tisa mchana akiwa na
wenzake watatu walipokuwa wakichunga ng’ombe.
Alisema
waliona kitu kama kifuniko cha mpira ambacho kilikuwa kimefungwa na
kuanza kurushiana na wenzake, Charles Ngine, Baraka Silonga na
Long’otuti Petro na ghafla kililipuka.
Alisema mwenzake, Petro alijeruhiwa kichwani huku ng’ombe watatu pia wakijeruhiwa na kitu hicho.
Kaka
wa Lowassa, ambaye anamtunza hospitalini hapo, Maige Kivuyo alisema
tukio hilo lilitokea eneo la Elperera, Kata ya Sepeko wilayani Monduli.
“Alikuwa na wenzake wanachezea kwa kurushiana kitu ambacho tunadhani ni bomu na ndipo kililipuka,” alisema.`
Kivuyo
alisema eneo hilo ni la Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lakini huwa
wanaruhusiwa kuingiza mifugo yao mara baada ya mazoezi kumalizika.
Muuguzi
wa zamu wa wodi namba mbili, kitengo cha mifupa, alipolazwa Lowassa,
Deodata Mahela alisema mtoto huyo amekatika vidole tisa na amebaki na
kimoja cha mkono wa kushoto.
“Hivi
sasa anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu, kwani pia alikuwa
amepata majeraha mengine kidogo pembeni ya kifua,” alisema Mahela.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Erick Komba alisema jeshi halina taarifa za tukio hilo.
“Tutachunguza mara moja na kupata ukweli wa taarifa hiyo,” alisema.
Na Mussa Juma, Mwananchi