Zikiwa zimechezwa mechi 20 za ligi ya England timu mbili za juu kwenye ligi hiyo zimeonyesha jinsi ambavyo upinzani na ushindani kwenye ligi hii inayopendwa karibu kila kona ya dunia ulivyo wa nguvu.
Kama leo hii ndio ingekuwa siku ya mwisho ambayo bingwa wa ligi hiyo angepaswa kuamuliwa basi hakuna shaka ingelazimu kwa mechi maalum ya kumpata bingwa kuandaliwa kwani hakuna tofauti yoyote katika vile vigezo vya kumpata bingwa ambavyo vinaonyesha nani yuko juu.
Timu zote hizi mbili zimejikuta zikiwa zimefungana kwenye rekodi zote muhimu kuanzia pointi , magoli ya kufunga na kufungwa , tofauti ya mabao kwa jumla , idadi ya mechi ambazo timu zote imeshinda , mechi zilizotoka sare na mechi ambazo timu hizi zimefungwa .
Chelsea na Manchester City zote hadi sasa zimetimiza idadi ya pointi 46 huku zikiwa na tofauti ya mabao ambayo ni +25 baada ya kila mmoja kufunga mabao 44 na kuruhusu kufungwa mabao 19 .
Msimamo wa Ligi ya England kwa timu mbili za juu.
Timu | Mechi | Ushindi | Sare | Kufungwa | Magoli+ | Magoli- | GD | Pointi | |
1 | Chelsea | 20 | 14 | 4 | 2 | 44 | 19 | 25 | 46 |
2 | Manchester City | 20 | 14 | 4 | 2 | 44 | 19 | 25 | 46 |
Mara ya mwisho kwa rekodi kama hizi kuonekana ilikuwa msimu wa mwaka 2004 wakati ambapo Arsenal na Manchester United walipokuwa wamefungana kwenye rekodi zote japo Arsenal waliishia kutwaa ubingwa mwishoni mwa msimu huo.
Cha kushangaza ni kwamba rekodi hizi zinaonekana kwenda hata kwa wachezaji binafsi ambapo washambuliaji wa timu hizi mbili Sergio Kun Aguerro na Diego Costa nao wamefungana kwenye idadi sawa ya mabao ambayo wamefunga kwenye mechi walizocheza msimu huu wakiwa na mabao 14 kila mmoja .
Kwa jinsi msimamo wa ligi ya England ulivyo hivi sasa Chelsea wanaonekana wanaongoza ligi lakini ni kwa sababu ya herufi C ambayo iko mbele ya herufi M kwenye majina ya timu hizi hali inayoonyesha kuwa tofauti pekee baina ya Chelsea na Man City hadi sasa ni herufi C na M .
0 Comments