UWEZO
wa Bwawa la Mabayani linalotegemewa kama chanzo cha maji ya kunywa na
wakazi zaidi ya laki mbili wa jijini Tanga umeendelea kupungua kutokana
na ogezeko la kasi la shughuli za kijamii na kiuchumi zinazoambatana na
uharibifu wa mazingira kwenye Mto Zigi.
Mwendelezo wa vitendo hivyo bila kuwepo
jitihada za makusudi za serikali na wadau kuwekeza ili kuvidhibiti hivi
sasa unaongeza hofu ya uwezekano mkubwa wa kukosekana kwa huduma ya
uhakika ya maji katika miaka michache ijayo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka jijini Tanga (UWASA), Farles
Aram mwishoni mwa wiki katika mahojiano maalum na mwandishi kuhusu
uhakika wa upatikanaji endelevu wa huduma hiyo katika miaka mitano
ijayo.
Aram alisema katika miaka ya hivi
karibuni kumeibuka kasi ya mwendelezo wa makusudi wa shughuli za kilimo
cha mazao ya chakula na biashara ambacho huambatana na matumizi ya
mbolea za viwandani na ukataji wa miti ili kupata magogo.
“Shughuli nyingine ni ukataji wa miti
hasa ile iliyoko katika uwanda wa juu ya milima ya Amani unakopita mto
Zigi ambao ndiyo pekee unaotegemewa na Uwasa kujaza bwawa la Mabayani”,
alisema.
Alisema athari ya jumla ya vitendo hivyo
ni kusababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo na viambatasumu kuelekea
mtoni na baadae kuvutwa taratibu hadi ndani ya bwawa na hivyo kupunguza
kina pamoja na uwezo wake wa kuhifadhi maji siku hadi siku.
“Pamoja na kwamba kazi ya mitambo yetu
ni kusafisha maji hasa kabla ya kumfikia mwananchi lakini katika miaka
ya hivi karibuni tumekuwa tukipata maji yenye rangi zaidi ya ile ya
kawaida hatua inayoilazimu mamlaka kupata hasara kubwa ya kununua dawa
nyingi zaidi ili kuyasafisha… kitendo hicho nacho kina athari kwetu
kwasababu matumizi ya dawa nyingi yanapunguza kiasi cha maji
yanayotarajiwa kwenda mjini kwa matumizi”, alisema.
Akizungumzia kazi ya ukatiji wa miti
alisema pamoja na kuchochea ukuzaji wa uchumi wa wananchi na pato la
serikali nayo inaathari kwenye ustawi wa uendelevu wa huduma hiyo jijini
Tanga.
“Ukataji wa miti nao husababisha
uchafuzi kwa kuwa majani makavu yanayopukutika huingia mtoni na
kusababisha kuoza ambako huzalisha harufu na rangi isiyo ya kawaida
kwenye maji yanayoingia Mabayani”, alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema ili
kuwezesha mamlaka kuwa na uhakikika wa kuendeleza shughuli zake ni vema
serikali na wananchi kushirikiana na Uwasa kudhibiti kasi ya ongezeko la
shughuli hizo.
“ Unajua tafsiri ya jumla ya shughuli
zinazoendelezwa huko juu mlimani endapo hazitadhibitiwa haraka ni kwamba
wakati wowote kuanzia sasa kutakapotokea ukame wa muda mrefu ina maana
maji yatakayoingia bwawani yatakuwa kidogo sana … na kwa hali kama hiyo
ni dhahiri kwamba upo uwezekano mkubwa wa kupungua au kukosekana kabisa
kwa huduma hiyo punde”, alisema.
Aidha aliongeza, “Kwa sasa si rahisi
sana Uwasa kujihakikishia uhakika endelevu wa upatikanaji wa huduma ya
majisafi kwasababu mamlaka haihusiki moja kwa moja na utunzaji wa
mazingira, ingawa imeanza kututumia rasilimali kidogo ku ‘mobilize’
vikundi vya wanavijiji kuhifadhi mazingira lakini nguvu zaidi na
ushirikiano wa serikali na wadau wengine vinahitajika”, alisema.
Alisema wakati umefika kwa serikali na
watunga sera kuangalia uwezekano wa kuondoa ukinzani katika masuala yote
ya kisheria hasa yanayohusu rasilimali za ardhi, maji, mazingira na
madini kwakuwa hizo zinagusa uhai wa mwananchi moja kwa moja.
Hata hivyo, kulingana na matokeo ya
utafiti wa Arab Contractors wa mwaka 2009 umeonyesha kwamba kina cha
Bwawa hilo kimepungua kwa asilimia 38.
Aidha, takwimu za hivi karibuni za UWASA zinazobainisha kuhusu tatizo
zimesisitiza kwamba uwezo(kina) wake umeshuka kutoka Cubic Mita za
ujazo Milioni 7.7 wakati lilipojengwa hadi kufikia Cubic mita za ujazo
milioni 5.6 ilipofika mwishoni mwa mwaka 2012.Mamlaka katika taarifa yake hiyo imesema kwa sasa uwezo wa bwawa hilo unaendelea kupungua siku hadi siku kwasababu ya mwendelezo usio na kikomo wa shughuli za uchafuzi na uharibifu wa mazingira juu mlimani.
0 Comments