Katika siku za hivi
karibuni kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao
mbalimbali ya kijamii kwamba shindano la urembo nchini maarufu kwa jina
la Miss Tanzania limefunguliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na
kwamba Kampuni ya Lino International Agency LTD ambayo ni waendeshaji wa
shindano hilo imewataka mawakala wake kuanza maandalizi ya shindano
hilo.
Taarifa hizo za
kufunguliwa shindano hilo zilienda mbali kwa kueleza kwamba mawakala
wametumiwa kalenda ya mashindano hayo kwa mwaka huu.
Baraza linapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
1. Wananchi wapuuze
taarifa hizo kwani kusimamishwa kwa shindano la Miss Tanzania bado kuko
palepale kama ilivyoelezwa katika barua ya BASATA ya tarehe 22/12/2014
waliyoandikiwa Lino International Agency LTD ambayo pamoja na mambo
mengine iliwataka warekebishe kasoro kadhaa zilizojitokeza.
Walisimamishwa kwa misimu miwili ya mwaka 2015 na 2016 ili kujipanga
upya na kurekebisha kasoro husika.
2. BASATA kama msimamizi
na mratibu mkuu wa sekta ya Sanaa nchini ndilo lililolisimamisha
shindano hilo baada ya kubaini mapungufu mengi. Kusimamishwa kwa
shindano hili ilikuwa ni kwa njia ya kuufahamisha umma na kwa maana hiyo
kama shindano litafunguliwa njia hiyo-hiyo ya kutoa taarifa kwa umma
itatumika na si vinginevyo.
3. BASATA linatoa wito
kwa Lino International Agency LTD kutumia muda wake mwingi kufanyia
marekebisho mapungufu yaliyojitokeza ili mashindano haya yatakaporejea
yawe na mikakati na hadhi kuliko ilivyo sasa.
4. Aidha, Baraza
linawataka wasanii na wadau wote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu
zilizopo katika kuendesha shughuli za Sanaa sambamba na kufuata mifumo
sahihi ya mawasiliano.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
0 Comments