Tume ya uchaguzi nchini
Tanzania NEC, imetoa ufafanuzi juu ya suala la upigaji wa kura ya maoni
ya Katiba Inayopendekezwa kuchanganywa na uchaguzi mkuu na kusema kuwa
mambo hayo hayatafanyika kwa pamoja.
Mwenyekiti wa Tume hiyo
Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa mpaka sasa tume haijaamua ni
lini kura ya maoni itafanyika ila kwa sasa wanachofanya ni kuendelea na
uandikishaji wa Daftari la mpiga kura katika Mikoa iliyobaki.
Jaji Lubuva ameongeza
kuwa uchaguzi mkuu wa Rais utakuwepo kama ulivyopangwa kuwa ni katika
juma la mwisho la mwezi Oktoboa ambapo tayari uandikishaji wa daftari la
mpiga kura kwa mfumo wa BVR, utakuwa umekamilika.
Mwenyekiti huyo amesema
kuna upotoshaji unaofanywa na baadhi ya vyama vya siasa kwamba tume
imesema itachanganya upigaji wa kura ya maoni na uchuguzi mkuu na kusema
kuwa suala hilo halina ukweli wowote.
Lubuva amesema kuwa
hakuna sheria inayokataza kuchanganywa kwa zoezi hilo kwa wakati mmoja
lakini amesema kufanya hivyo kuna changamto nyingi ambazo zitaweza
kuharibu chaguzi hizo ikiwa ni pamoja na jinsi ya kufanya kampeni.
Aidha jaji lubuva
amekanusha tuhuma za kwamba tume hiyo imeanza uandikishaji katika mikoa
ambayo ni ngome ya chama Tawala ili kuhujumu vyama vya upinzani na
kusema tuhuma hizo si za kweli na ni upotoshaji na kusema kuwa tume
inafanya kazi kwa misingi na taratibu ilizojipangia.
Ameongeza kuwa kwa
kuanza mikoa ambayo yamechagua kwa ajili ya zoezi hilo kunatokana na
idadi ya watu katika mikoa hiyo kuwa ndogo hivyo kutokana na vifaa vya
kujiandikishia kuwa vichache ndio maana wakaanzia mkoa wa Njombe na sasa
wataendelea na mikoa mingine ya Iringa, Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Hatua hiyo inafuatia
kutokana na shutuma za vyama vya siasa ikiwemo Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo CHADEMA ambapo naibu Katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Zanzibar Salumu Mwalim, amesema kuwa tume ya taifa
Uchaguzi (NEC) isije ikathubutu kuuchezea uchaguzi mkuu kwa kuuchanganya
na kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa wakithubutu hawata shiriki
uchaguzi mkuu Oktoba.
Akizungumza na mamia ya
wakazi wa mji wa Njombe Mwalimu amesema kuwa chama hicho hakita shiriki
uchaguzi mkuu kama kutatokea uchaguzi mkuu kuchanganywa na kura ya maoni
ya Katiba Pendekezwa.
Amesema kuwa kitu hicho
kitavunja historia ya nchi na dunia kwani hakijawahi kutokea ulimwenguni
pote na kuwa itakuwa ni Tanzania pekee kupiga kura mbili tofauti kwa
wakati mmoja.
0 Comments