Taarifa zilizotua kwenye
dawati la gazeti hili zinadai kuwa, wale wamama wa mjini ambao walikuwa
mashosti hadi kufikia hatua ya kusema ni kama ndugu, mama wa aliyekuwa
staa wa Bongo Movies, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa na mama wa
mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’, Lucresia Karugila, sasa kimenuka!
DALILI KUWA PAKA NA CHUI
Chanzo chetu cha
kuaminika kilidai kuwa, dalili za wawili hao kuelekea kugeuka kuwa paka
na chui zilianza muda mrefu lakini hali ikazidi kuwa mbaya Siku ya
Kumbukumbu ya Kifo cha Kanumba, Aprili 7, mwaka huu alipokuwa akitimiza
miaka mitatu kaburini.
CHANZO NI LULU
Ubuyu ulidai kwamba,
siku ya kumbukumbu ya kifo cha Kunumba, Mama Kanumba alimtuhumu Lulu
kutotoa ushirikiano na kufikia hatua ya kutoa maneno makali zaidi
yaliyomkera mama Lulu.
Mama wa aliyekuwa staa wa Bongo Movies, marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa.
MAMA KANUMBA NA SMS MBAYA KWA MAMA LULU
Ilidaiwa kwamba, siku ya
kumbukumbu ya kifo cha Kanumba, mama Kanumba alimtumia mama lulu sms
mbaya ya kejeli (kuiandika hapa siyo busara) ndipo mama Lulu
‘alipofyumu’ na kuona kwa hali hiyo bora kama mbwai na iwe mbwai.“Ile
sms mama Kanumba alimtumia mama Lulu siku ile (Aprili 7) majira ya saa
11:00 alfajiri.
HAIKUWA YA KIUNGWANA
“Kwa kweli ilikuwa
meseji mbaya mno. Alikuwa akimuagiza mama Lulu amuamshe Lulu kwa ajili
ya kwenda kaburini kwa Kanumba lakini haikuwa ya kiungwana.“Hata hivyo,
ukweli mama Lulu alitumia busara kwa kutomjibu lakini akadhamiria
kuchukua hatua za kisheria,” alidai mtoa ‘ubuyu’ huyo.
Enzi za ushosti wao.
Ilizidi kudaiwa kwamba,
wakati mama Lulu akitafakari sababu ya shosti wake huyo ambaye walikuwa
wakitembea mjini kama kumbikumbi kumtumia sms hiyo, akashangaa kusoma
tena kwenye gazeti mama Kanumba akimpa vipande vyake Lulu, jambo
lililozidi kumchefua mama Lulu.
KUBURUZANA KORTINI?
“Kimsingi hali ni mbaya
sana sasa hivi, inavyoonekana mama Lulu kamchoka mama Kanumba na anataka
kuchukua hatua zaidi ikiwemo kuburuzana kortini,” alidai sosi huyo.
MAMA LULU AFUNGUKA
Baada ya kunyetishiwa
ishu hiyo, gazeti hili lilimtafuta mama Lulu ambapo alipopatikana
alikiri kupokea ujumbe na kwamba hali ni mbaya sana.“Nimeumizwa sana na
sms ya mama Kanumba lakini siwezi kuwapa kwa sababu nataka kuifanyia
kazi,” alisema mama Lulu.
Mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’.
MAMA KANUMBA VIPI?
Kwa upande wake mama
Kanumba aliendelea kusisitiza kuwa yeye ataendelea kumlilia mwanaye na
hana mpango na familia hiyo ya Lulu.“Mimi kwa upande wangu nitamlilia
mtoto wangu mpaka siku ya kufa kwangu lakini kinachoniuma ni Lulu
kufanya sherehe ya mdogo wake siku ya kumbukumbu ya mwanangu.
“Jamani hata kama mtu ana roho gani, hawezi kufanya hivyo,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu sms
aliyomtumia mama Lulu na kwamba mama huyo yupo mbioni kumchukulia hatua
za kisheria hakuwa tayari kuzungumza chochote.
0 Comments