Maajabu! Dada mmoja
msaidizi wa kazi za ndani maarufu kama Hausigeli, aitwaye Sophia Omari
(24) ambaye ndugu zake walitangaza kuwa alifariki kwa kunywa sumu,
aliibuka nyumbani kwao mtaa wa Tuelewane, Kihonda mjini Morogoro Jumanne
wiki hii wakati wanandugu wakijiandaa kwa ajili ya mazishi ya mwili
wake, Ijumaa lina mkasa kamili.
Sophia aliyetinga
nyumbani hapo akiwa kwenye bodaboda pamoja na babu yake, alisababisha
waombolezaji waliojitokeza msibani hapo, kutimua mbio kwa kutokuamini
walichokiona mbele yao.Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo la aina
yake, awali Sophia alikuwa akiishi kwenye nyumba aliyopangiwa na
mwanaume mmoja mume wa mtu aliyezaa naye, lakini baada ya mke wa mume
huyo kujua na kwenda kumfanyia vurugu, binti huyo alikimbilia Mazimbu
kwa dada yake ambako alikuwa akifanya kazi za ndani kwa majirani.
Babu wa binti huyo
ambaye wazazi wake walifariki akiwa na umri mdogo, Juma Sigwa alisema
Sophia alilelewa na bibi yake lakini naye alipoaga dunia, alimchukua na
kumlea yeye kabla ya kumfukuza nyumbani kufuatia mabadiliko ya tabia
yake.
Ndugu wa karibu wa Sophia Omari akihojiwa.
“Jana (Jumatatu)
nimepokea meseji kutoka kwa Tausi kwamba Sophia kanywa sumu, kafa
tukaangua vilio, baadaye tukafunga turubai huku baadhi ya majirani
wakienda kuchimba kaburi, ndugu wa mbali wamefika, leo nikaamua kwenda
Mazimbu kuuchukua mwili.“Cha ajabu, nafika Mazimbu namkuta Sophia yuko
jikoni anapika uji, nikashangaa, baadaye nikawajulisha wenzangu,
wakaniambia nimlete msibani, nikakodi bodaboda na kuja naye, watu
walipomuona wakatimua mbio kwa woga,” alisema mzee huyo.
Inadaiwa kuwa Sophia na
dada yake Halima wanaoishi pamoja Mazimbu, wote hawana simu, isipokuwa
walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kupitia kwa jirani yao, namba ambayo
ndiyo ilituma sms kwa ndugu kuwafahamisha kuhusu kufariki kwa msichana
huyo.
Wananchi wakifuatilia tukio hilo la kushangaza.
Sophia mwenyewe
akizungumzia juu ya sakata hilo, alisema ni uchuro unaoendelea katika
maisha yake kwani amekuwa ni mtu wa majanga.“Tukio hili ni muendelezo wa
majanga ninayoendelea kuyapata, wazazi wangu walikufa nikiwa darasa la
tatu, ndugu wakashindwa kunisaidia, nikaacha shule darasa la tatu,
nikaishi na bibi mzaa mama naye akafa, babu akanichukua na baadaye
kanifukuza, nikiwa na umri wa miaka 16 nikatembea na mume wa mtu anaitwa
Seif, akanipa mimba, akanipangia chumba nikajifungua mtoto Khadija,”
alisema binti huyo.
Alisema mwaka jana mtoto
wake alivyotimiza miaka miwili, mke wa Seif alijua na kuanza kumtafuta
hadi akampata na kumfanyia vurugu kubwa, kabla ya kesho yake mumewe
kufika hapo na kumchukua mtoto wake ambaye alimpeleka Dodoma kwa mama
yake mzazi ambako hajaonana naye tena wala kuwasiliana maana alibadili
namba.
0 Comments