Katika
hali isiyokuwa ya kawaida Mbunge wa Bariadi Mgaharibi mkoani Simiyu Andrew Chenge (CCM)amenusurika kipigo kutoka kwa wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) mkoani Simiyu baada ya kupita katika ofisi zao akitoka
kwenye mkutano wake.
Tukio
hilo lilitokea jana majira ya saa moja na nusu usiku baada ya vyama
hivyo CCM na Chadema kumaliza mikutano yao ya hadhara iliyokuwa
ikifanyika katika maeneo tofauti mjini Bariadi hali ambayo ilisababisha
kuwepo kwa vurugu hizo.
Hali ya hewa ilibadilika baada ya wafuasi wa CHADEMA kuzuia msafara wa Mbunge huyo na kuanza kurushia mawe magari yaliyokuwa
katika msafara huo ambapo mmoja wa makada wake alijulikana kwa jina la Ahmed
Ismail alilazimika kurusha risasi tatu hewani ili kuwatawanya watu waliokuwa
wameziba njia.
"Hali
hiyo imetokea baada ya msafara wa Chenge kuondoka katika mkutano wao uliokuwa
katika kijiji cha Isanga jimboni kwake, ambapo wakati wakipita katika ofisi za
Chadema Mkoa zilizoko barabara kuu ya Bariadi-Shinyanga walianza kuzomewa na
wafuasi wa CHADEMA",walieleza mashuhuda wa tukio hilo.
Akidhibitisha
kuwepo kwa tukio hilo Kamishena Msaidizi wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Gemini
Mushi alisema kuwa vyama hivyo baada ya kumaliza mikutano yao Chadema walianza
safari ya kuelekea katika ofisi zao huku msafara wa mbunge ulikuwa ukirejea .
Kamanda
alibainisha kuwa baada ya msafara huo kufika katika eneo la ofisi ya Chadema
walikuta kundi kubwa la watu wakishangilia na ndipo mbunge huyo akashuka kwenye
gari na kuanza kucheza nao wakati wakiendelea kushangilia walisikia sauti
ikisema rusha mawe hali ambayo ilisababisha mbunge huyo kukimbilia kwenye gari.
Mushi
alisema kuwa baada ya wafuasi hao wa Chadema kurusha mawe wakishambulia gari
alilokuwa amepanda mbunge huyo, ndipo risasi tatu zilirushwa hewani kwa ajili ya
kuwatawanya na kufanikisha wafuasi hao kukimbia na kUtawanyika.
Mushi
alieleza kuwa baada ya tukio hilo wafuasi wote wa vyama viwili walikimbilia
kituo cha polisi Bariadi kutoa taarifa, ndipo askari wake walifika eneo la
tukio na kuanza uchunguzi.
Alisema
risasi hizo zilizorushwa na mfuasi huyo wa Chenge zilikuwa na lengo la
kuwatawanya wafuasi hao ambao alisema walianza kuleta vurugu, huku akieleza
kuwa siLaha hiyo ni bunduki aina ya bastola.
Kamanda
huyo alieleza kuwa uchunguzi bado unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo cha
vurugu hizo, huku akieleza kuwa hakuna majeruhi na hakuna mtu anayeshikiliwa na
jeshi hilo.
Mashududa wa tukio hilo
Baadhi
ya mashuda wa tukio hilo wameeleza kuwa baada ya kukutana hapo wafuasi wa vyama
hivyo waliaza kurushiana mawe na ndipo mbunge kukimbilia kwenye gari na baadhi
ya wafuasi wa Chadema walianza kuirushia mawe gari aliyokuwa amepanda mbunge
hali ambayo iliwalazimu kurusha risasi mmoja wa makada wa CCM waliokuwa katika
gari hilo.
“Tulishangaa
kuona wafuasi wa CCM na Chadema kuanza kushambuliana kwa mawe baada ya watu wa
CCM kutokea katika mikutano yao ya hadhara na kufika katika maeneo ya Salunda
wafuasi wa ccm na Chadema walikutana na kuanza kushambuliana kwa mawe baadaye
tulisikia risasi zinalia”Alisema Nkuba Majaliwa shuhuda wa tukio hilo.
Heche asimulia.
Kiongozi
wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema John Heche alisema kuwa chama cha
CCM walipita katika ofisi za chadema wakakuta viongozi wanafanya mikutano ya
ndani ambapo msafara wa CCM ulifika katika ofisi hiyo na kuanza kupiga muziki
hali ambayo ilipelekea baadhi ya viongozi kutoka kwenda kuwazuia kwa madai ya
kupunguza muziki.
“Msafara
wa CCM ulifika katika ofisi ya Chadema baada ya kutoka katika mikutano yao
walipofika katika maeneo ya ofisi zetu walisimamisha magari yao na kuanza
kupiga muziki na wafuasi wao waliteremka kwenye magari na kuanza kucheza hali
ambayo tulienda kuwazuia kwa misingi ya kupunguza muziki kwani tulikuwa tunafanya
kikao cha chama lakini walikaidi na ndipo wafuasi wetu walianza kuwashambulia
kwa mawe hali ,wao walirusha risasi hewani kwa ajili ya kutawanya”Alisema
Heche.
Kwa
upande wake katibu wa umoja wa vijana wa CCM wilaya ya Bariadi Sai Samba alieleza
kuwa baada ya kufika katika eneo la ofisi ya Chadema walikuta kundi kubwa la
vijana wakiwa barabarani ambapo walipofika wakazuia msafara na ndipo kundi la
vijana walianza kumrushia mawe mbunge wao.
Alisema baada ya kuona hali hiyo
mmoja wa makada wao aliamua kurusha risasi hewani ili wafuasi hao wasimdhuru
Mbunge huyo ambaye gari lake lilikuwa likishambuliwa kwa mawe.
“Baada ya kufika katika maeneo ya ofisi ya Chadema tulikuta watu ambao walikuwa
wamejiandaa kwa ajili ya kuushambulia msafara wa mbunge Andrew Chenge na
tulipofika pale walianza kucheza na mbunge akateremka kwenye gari na kuanza
kucheza nao lakini ilisikika sauti ikiamuru vijana kurusha mawe na ndipo
walianza kurusha mawe hali iliyopelekea kurusha risasi hewani”,alisema Samba
Walipotafutwa
kuongelea
suala hilo la kurusha risasi hewani Mbunge wa Bariadi Magharibi na
kada huyo wa CCM Ahmed Ismail hawakupokea simu lakini baadaye mbunge
huyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo bali jeshi la polisi ndilo
linaweza kuzungumzia suala hilo.
0 Comments