Mbunge
wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila, amepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kujibu shtaka la kutumia
lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Kafulila alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:00 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mbele
ya Hakimu wa Mahakama hiyo, David Ngunyale, Wakili wa Serikali,
Maryasinta Lazaro, alidai kuwa Mbunge huyo alitenda kosa hilo Agosti
Mosi, mwaka 2013, katika Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani
Kigoma.
Wakili
huyo alidai kuwa Mbunge huyo alimtolea maneno ya matusi Nyembo kuwa
hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho
kingesababisha uvunjifu wa amani.
Wakili
Lazaro, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo namba CC 6/2015 umekamilika
na kuomba kupangwa tarehe nyingine ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Ngunyale alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, mwaka huu.
Wakili
wa Mbunge huyo, Danieli Rumenyela, aliomba Mahakama hiyo kumpunguzia
mteja wake masharti ya dhamana ili kumalizia vikao vya Bunge ambavyo
vinatarajia kuanza mwezi ujao.
Hata
hivyo, Kafulila alikana shtaka hilo na kukidhi masharti ya dhamana
ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa
Ofisa Mtendaji wa Kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh.
milioni mbili kisha kuachiwa.
Kafulila alidhaminiwa na Diwani wa Kata ya Katubuka (Chadema), Moses Bilantanye.
Kabla
ya kufikishwa mahakamani jana, Mbunge huyo alikuwa nje kwa dhamana
ambayo alipewa na askari wa kituo cha Polisi Kati baada ya kudaiwa
kumtukana Mkuu huyo wa wilaya.
Jana
Kafulila aliporipoti katika kituo hicho saa 1:00 asubuhi, alipelekwa
mahakamani hapo baada ya Mwanasheria wa Serikali kuandaa mashtaka dhidi
yake.
Hali Ilivyokuwa
Nje
ya mahakama hiyo walifurika wafuasi wa vyama vya siasa vya upinzani
wakiwamo madiwani, wapambe wa mbunge huyo ambaye ndiye aliyeibua bungeni
sakata la uchotaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia
ulinzi ulikuwa umeimarishwa katika Mahakama hiyo, ambako pia kulikuwa
na usikilizaji wa kesi za mauaji zilizokuwa zinasikilizwa na Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora.
0 Comments